Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Rasoul Razi, mbunge wa zamani wa Bunge la Iraq, katika mahojiano aliyofanya, amesisitiza kuendelea kwa utawala wa Marekani juu ya maamuzi ya kisiasa na sekta ya kijeshi ya Iraq. Aliongeza kuwa mamlaka ya Iraq bado hayajakamilika kutokana na utawala wa Washington na uingiliaji wake katika maamuzi ya nchi hiyo.
Razi alisema kuwa; kuondoka kwa majeshi ya Marekani katika ardhi ya Iraq hakumaanishi kuwa nchi hiyo imepata mamlaka kamili ya kujitawala, bali maamuzi mengi bado yanaendelea kufuata matakwa ya serikali ya Marekani. Alifafanua kuwa jambo hilo linajidhihirisha zaidi kwa Washington kumweka mwakilishi wake, Tom Barrack, nchini Iraq.
Aliongeza kuwa tatizo kubwa ni kushindwa serikali ya Iraq kujinasua kutoka katika mfumo wa maamuzi unaoongozwa na Marekani. Hali kadhalika, Wizara ya Ulinzi ya Iraq imeshindwa kuchukua hatua kwa mujibu wa matakwa yake yenyewe katika kufikia makubaliano na mikataba na nchi nyingine, kwa lengo la kuzipatia taasisi za usalama silaha zinazohitajika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba utawala wa Marekani na udhibiti wake wa kisiasa juu ya Iraq bado unaendelea kuwepo.
Aidha, alisema kuwa serikali bado haijalipa uzito unaostahili suala la udhibiti wa Marekani katika maamuzi ya Iraq na upatikanaji wa silaha kwa taasisi za usalama. Alionya kuwa huenda bajeti inayotengwa kwa ajili ya Wizara ya Ulinzi isiwe katika kiwango kinachohitajika ili kuwezesha upatikanaji wa silaha na kufanyika kwa maboresho ya taasisi za usalama, pamoja na kuziba mapungufu yaliyopo katika mifumo ya ulinzi wa anga.
Maoni yako